MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara wamejiweka katika wakati mgumu wa kusonga mbele baada ya kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Zanaco FC katika mechi ya Klabu Bingwa Afrika iliyopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.
Winga Simon Msuva ndiye aliyefunga kwa upande wa Yanga baada ya kumalizia pasi
iliyoanzia kwa Donald Ngoma na kisha Justine Zulu katika dakika ya 38.
Bao hilo la Msuva ambaye ni kinara wa kupachika mabao kwenye Ligi Kuu liliifanya Yanga
iende mapumziko ikiwa mbele kwa 1-0, lakini vinara hao wa Ligi Kuu ya Zambia walimwaga
‘pilau’ la vijana wa Mzambia George Lwandamina kipindi cha pili kupitia kwa Mghana wao,
Attram Kwame.
Kwame aliisawazishia Zanaco baada ya kupiga shuti kali lililomshinda kipa wa Yanga,
Deogratius Munishi " Dida" akiunganisha krosi ya Ernest Mbwewe katika dakika ya 77.
Mabingwa hao watetezi wa Kombe la FA ndio walikuwa wa kwanza kufanya shambulizi kwa
wapinzani wao, lakini mshambuliaji Ngoma alipiga shuti pembeni na kupoteza nafasi hiyo ya
wazi ndani ya 18.
Dakika ya 12, Zanaco ilijibu shambulio hilo kupitia kwa Kwame, lakini kipa wa
Yanga, Dida aliruka na kupangua shuti la straika huyo kabla ya kudaka tena
shuti la Richard Kasonde dakika ya 21.
Yanga ilipoteza nafasi nyingine kupitia kwa Msuva baada ya kupiga mpira nje
kwa kichwa na kuharibu krosi safi aliyopigiwa na Hassan Kessy katika dakika
ya 31.
Thabani Kamusoko alimpa pasi Ngoma, lakini Mzimbabwe huyo ambaye
alikuwa majeruhi kwa zaidi ya mwezi, alipiga tena shuti pembeni na kupoteza
nafasi nyingine ya kuwanyanyua mashabiki wa Yanga huku mabeki wa Zanaco
wakiwa wamepoteana katika dakika ya 35.
Zanaco ilianza kwa kasi kipindi cha pili, lakini mshambuliaji wake Saith Sakala
alishindwa kuunganisha krosi ya Augustine Mulenga na kumfanya Dida kuwahi
kudaka mpira uliotua chini ukitokea kifuani.
Timu hizo zitarudiana Jumamosi mjini Lusaka, Zambia na mshindi wa jumla atatinga hatua
ya 16-Bora ya michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), huku
itakayotolewa ikitinga Kombe la Shirikisho.
Yanga: Deogratius Munishi "Dida", Hassan Kessy, Mwinyi Haji, Vincent Bossou, Nadir
Haroub "Cannavaro", Kelvin Yondani, Simon Msuva, Justine Zulu/ Deus Kaseke (dk. 83),
Donald Ngoma/ Emmanuel Martin (dk. 58), Thabani Kamusoko/ Juma Mahadhi (dk. 60) na
Obrey Chirwa.
Zanaco: Racha Kola, Zimiseleni Moyo, Chongo Chirwa, Saith Sakala/ Kennedy Musonda(dk.
69), Ziyo Kola, Taonga Mbwembya, Richard Kasonde, Attram Kwame, Augustine Mulenga,
Ernest Mbwewe/ Ayubu Lyanga (dk. 85) na George Chilufya.
0 comments:
Post a Comment