Prof; Joyce Ndalichako
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imesema kuwa tangazo lao la mwanzo halikusoma ama halikusema kama kuna wanafunzi wasio na sifa katika vyuo bali liliwataka baadhi ya wanafunzi ambao taarifa zao hazijakaa vizuri wakahakiki.
“Tangazo letu la mwanzo halikusoma ama halikusema, kama kuna wanafunzi wasio na sifa katika vyuo, bali lilisema wanafunzi wafuatao taarifa zao hazijakaa vizuri kwa hiyo waka hakiki, na watapohakiki kila kitu kitakuwa sawa,”
Taarifa ya tume imesema kuwa uhakiki wa ubora wa wanafunzi wa elimu ya juu hufanyika kwa mujibu wa kifungu 5(1)(b)(c) cha Sheria ya Vyuo Vikuu Sura ya 346 ya Sheria za Tanzania.
Katika kutekeleza jukumu hili Tume ilianza zoezi la uhakiki kuanzia mwezi Agosti 2016. Hadi kufikia Februari 2017 zoezi hilo lilikuwa limekamilika kwa vyuo 67 kati ya 84 vinavyotoa shahada ya kwanza, taarifa hiyo imefafanua.
Hii ni mara ya kwanza uhakiki wa sifa za wanafunzi wa vyuo vyote nchini kufanyika kwa wakati mmoja .
Lengo la uhakiki lilikuwa kujiridhisha kuwa wanafunzi waliopo vyuoni ni wale waliodahiliwa kwa mujibu wa sheria na taratibu na kwamba wanakidhi vigezo stahiki.
Uhakiki ulifanyika kwa kulinganisha taarifa za TCU na zile zilizowasilishwa na vyuo. Uhakiki huo ulihusisha jumla ya wanafunzi 131,994 waliopo vyuoni kwa mwaka wa masomo 2016/17.
Baada ya kulinganisha orodha zilizowasilishwa na vyuo na ile ya TCU ilibainika kuwa wanafunzi 123,827 sawa na asilimia 93.8 wana sifa stahiki. Aidha jumla ya wanafunzi 8,167 sawa na asilimia 6.2 to walibainika kuwa na kasoro katika taarifa za sifa zao.
Kufuatia hali hiyo, Tume ilitoa taarifa kwa umma kuwaomba wanafunzi kurekebisha dosari hizo kwa kuthibitisha taarifa zao kupitia vyuo husika ifikapo tarehe 28 Februari 2017 ili kuweka kumbukumbu sahihi za mwanafunzi.
Hata hivyo imebainika kuwa taarifa hiyo imepokelewa kwa mtazamo na hisia tofauti na hivyo kusababisha mkanganyiko vyuoni. Umma unaarifiwa kwamba haikuwa nia wala lengo la Tume kusababisha mkanganyiko huo.
Kwa kuwa uhakiki wa sifa za wanafunzi ni kazi endelevu ya Tume na kutokana na maombi ya wadau mbalimbali, Tume sasa itaendelea kuwasiliana moja kwa moja na vyuo katika kukamilisha zoezi hilo.
“Hivyo wanafunzi wote waliokuwa wameorodheshwa katika taarifa iliyotolewa awali wanaombwa kuwa watulivu na kuendelea na masomo yao kama kawaida,” imeeleza taarifa hiyo.
0 comments:
Post a Comment