Mbunge wa Mikumi kwa tiketi ya CHADEMA, Joseph Haule maarufu Professor Jay ameeleza masikitiko yake baada ya nyumba yake kubomolewa bila ya yeye kupewa taarifa ili aweze kutoa mali zake kabla ya zoezi hilo.
Nyumba ya mbunge huyo ambayo kwa mujibu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imo ndani ya hifadhi ya barabara ipo eneo la Mbezi Luis jijini Dar es Salaam na ilibomolewa Septemba 29 mwaka huu.
Usiku wa kumkia leo kupitia ukurasa wake wa Instagram mbunge huyo amendika ujumbe mrefu akielezea namna ambavyo hajaridhishwa na zoezi zima la ubomolewaji wa nyumba yake, akisema kwamba TANROADS hawakutenda haki.
“Mimi ni mmoja wa wahanga wa hili zoezi la kubomolewa nyumba zetu huku Mbezi Kimara Tarehe 29/9/ 2017.
Jana nikiwa katika majukumu jimboni Mikumi Majira ya saa kumi mbili hivi jioni, nilitaarifiwa kwamba, watu wa Tanroads wakiwa wameambatana na grader mbili na magari mawili ya polisi (defenders) yenye askari waliokuwa na silaha mbalimbali za moto walikuwa wanabomoa nyumba yangu. (sijawahi kuumia kiasi hiki ),” aliandika Professor Jay.
Akiendelea kusimuliwa tukio hilo alisema, “Nimesikitishwa sana jinsi Tanroads wanavyoweza kujichukulia maamuzi bila ya kujali mhimili muhimu wa Mahakama wametoa maagizo gani. Na taratibu zilizotumiwa kubomoa nyumba yangu bila ya mimi na Tanesco kupewa taarifa saa kumi na mbili jioni (haukuwa muda wa kazi) na kubomoa huku Umeme ukiwa unawaka ni kitendo ambacho kwanza kina hatarisha maisha ya wabomoaji wenyewe, maisha ya familia yangu pamoja na majirani zangu , LIMENISIKITISHA zaidi.”
Mbunge huyo ameeleza TANESCO pia walishangazwa na uamuzi wa TANROADS kubomoa nyumba hiyo umeme ukiwa unawaka na hata walipomuuliza mbunge huyo kama aliweza kutoa mita ya umeme, aliwajibu kuwa hakuokoa kitu.
“… nyumba IMESHABOMOLEWA kabisa na sijaweza kuokoa kitu chochote na hata hiyo meter yenu mnayoiulizia mkaitafute kwenye kile kifusi cha nyumba yangu kilichokusanywa kwa pamoja na watu wa Tanroads,” hayo ni majibu ya mbunge huyo kwa TANESCO.
Nyumba hiyo na nyingine zimebomolewa ili kupisha upanuzi wa Barabara ya Morogoro.
0 comments:
Post a Comment