WASHAMBULIAJI Donald Ngoma na Amis Tambwe ambao juzi walianza mazoezi kwenye kikosi cha timu hiyo, jana waliongezewa dozi ya mazoezi na kocha wa timu hiyo, George Lwandamina.
Katika mazoezi ya juzi yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini, Ngoma na Tambwe walifanya mazoezi mepesi kwa usimamizi wa kocha msaidizi wa timu hiyo, Juma Mwambusi.
Katika mazoezi ya jana yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, wachezaji hao waliungana rasmi na kikosi cha timu hiyo na kuendelea na programu za kocha Lwandamina.
Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh aliiambia Nipashe jana kuwa wachezaji hao wanaendelea vyema na maamuzi ya kucheza au kutocheza mchezo wa kesho yamebaki kwa Kocha.
"Kocha ndiye atakayeamua nani wa kumtumia kwenye mchezo na Zanaco, lakini Ngoma na Tambwe wameungana na wenzao na wanaendelea na mazoezi ya pamoja japo wao wameongezewa kidogo mazoezi maalum," alisema Saleh.
Aidha, Lwandamina alisema anaendelea kuwaangalia kwa karibu wachezaji hao na mazoezi ya leo jioni ndiyo yatampa picha ya kikosi chake cha kesho.
"Ni mchezo mgumu dhidi ya Zanaco, lakini kila mchezaji kwangu ana nafasi ya kucheza kulingana na kiwango chake na mahitaji ya mchezo," alisema Lwandamina.
Yanga kesho itawakaribsha Zanaco kwenye Uwanja wa Taifa katika mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika.
0 comments:
Post a Comment