Malawi imetangaza kwamba imejiondoa kutoka kwa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2019 pamoja na michuano ya Ubingwa Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani ya 2018.
Taifa hilo limechukua hatua hiyo kutokana na matatizo ya kifedha pamoja na kukosa mkufunzi wa timu ya taifa.
Shirikisho la Soka la Malawi lilitoa taarifa baada ya kunyimwa idhini ya kumwajiri kocha kutoka nje na serikali ya nchi hiyo.
Shirika hilo lilitaka kumwajiri mkufunzi kutoka nje ya nchi ambaye angelipwa mshahara kwa ubia wa nusu nusu kati ya shirika hilo na serikali.
Baada ya mashauriano ya miezi kadha, serikali kupitia Wizara ya Michezo ilikataa pendekezo la shirikisho hilo kwa misingi ya kifedha.
Kamati kuu tendaji ya shirikisho hilo ndipo ikafikia uamuzi wa kuondoa taifa hilo kutoka kwa michuano hiyo ya ubingwa wa bara Afrika.
Timu ya taifa ya Malawi itaondoka rasmi kutoka kwa CHAN kufikia 31 Machi na kutoka AFCON kufikia 30 Aprili.
Malawi walikuwa wamepangiwa kucheza dhidi ya Madagascar mechi yao ya kwanza ya kufuzu kwa CHAN 2018, michuano ambayo imepangiwa kuanza Aprili.
Kadhalika, walipangiwa kucheza nyumbani na mshindi wa mechi kati ya Comoros na Mauritius 13 Juni mechi yao ya kwanza ya kufuzu kwa AFCON 2019.
Malawi imekuwa bila mkufunzi wa timu ya taifa tangu Septemba 2016 raia wa Burundi Nsanzurwimo Ramadhan alipowaongoza kwa mechi moja ambayo walishinda 1-0 dhidi ya Swaziland mechi ya kufuzu kwa AFCON.
Alikuwa amechukua usukani baada ya kufutwa kwa Ernest Mtawali Julai mwaka huo.
0 comments:
Post a Comment